Mbunge Innocent Bashungwa aijia juu Serikali sakata la Kahawa
Siku ya leo Nane Nane tusimsahau mkulima wa Kahawa. Kuna mambo manne ya msingi lazima Serikali iyatambue na kuyatenda.
Jambo la kwanza ni pro-poor tax and regulatory regime (mfumo wa kodi na rafiki kwa mkulima na kuondoa urasimu). Pamoja na Serikali kuondoa kodi kero 21 kati ya 27, bado kuna urasimu na usumbufu mkubwa kwa mkulima wa Kahawa. Kuondoa kodi kero hizo ni hatua ila 6 zilizobaki ziondolewe na kazi kubwa bado ipo kwenye urasimu.
Jambo la pili ni uzingatiaji wa ubora. Msingi mkubwa wa kupata bei ya juu ya Kahawa upo hapa. Namna pekee ya kupambana na suala la global supply and demand ya kahawa duniani na ushindani katika soko la dunia ni kujikita katika ubora wa Kahawa ya Tanzania. Hili ni jukumu hasa la Serikali, mkulima, vyama vya msingi, vyama vikuu vya ushirika, wenye viwanda vya kukoboa, bodi ya kahawa na tume ya maendeleo ya ushirika. Katika msimu huu wa Kahawa 2018 taasisi hizi zinazosimamia mnyororo wa thamani ya kahawa kuna hali ya kukosa umakini katika kusimamia mfumo mpya wa stakabadhi ghalani huku wakijaribu kusukuma gharama za uzembe wao kwa mkulima. HII SIYO SAWA hata kidogo.
Mkulima ana kosa gani katika hili? Karagwe ni mwezi sasa wakulima wengi wamepeleka kahawa zao kwenye vyama vya msingi bado wanasubiri malipo ya awali ya Tsh 1,000. Serikali ilishasema mkulima haihitaji kukopesha kahawa yake, kwamba atapokea malipo ya awali ndani ya siku chache. Kwanini sasa imekuwa mwezi mzima na ni nani amesababisha hali hii?
Kwanini hakuna anayejitokeza kuelezea ni nini kilitokea na kwa nini? Mnada wa Kahawa ni kila Alhamisi kule Moshi, kwanini taarifa muhimu juu ya hali ya mnada haitolewi kwa mkulima kila wiki baada ya mnada ili kuondoa tatizo la usiri (asymmetry of information)? Redio zipo, magazeti yapo, TV zipo, social media ipo- usiri ni wa nini?
Jambo la tatu ni responsibility ya Serikali kutoa maafisa ugani wenye maarifa ya kahawa na ujuzi wa kutosha, pembejeo za kutosha na kutolewa kwa wakati, magala na miundombinu inayozingatia kanuni na viwango kwenye mnyororo wa thamani ya Kahawa kuanzia shambani hadi mnadani, mikopo ya bei nafuu kupitia SACCOS ndani ya vyama vya msingi ikiwa ni mbadala wa BUTURA badala ya kutumia nguvu na msuli. Ili kumtoa mkulima wa Kahawa kwenye BUTURA inabidi kuweka utaratibu mbadala usioshurutisha mkulima.
Jambo jingine ni kutoa elimu na kuwa na pro-farmer regulatory environment. Mkulima jukumu lake ni uzalishaji na kuzingatia kanuni na viwango vya kulima kahawa iliyo bora. Tukifanya hivyo tutakuwa katika njia sahihi ya kumkomboa mkulima wa Kahawa.
Nawatakia Nane Nane Njema.
Innocent L. Bashungwa, MB- Karagwe.
No comments: