Header Ads

TAKUKURU KILIMANJARO WAMPANDISHA MAHAKAMANI OFISA UCHAGUZI.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kilimanjaro imemfikisha Mahakamani Mkuu wa kitengo cha uchaguzi katika Halmashauri ya wilaya ya Hai,Edward Ntakiliho pamoja na mfanyabiashara ,Oscar Kigumu kwa makosa mbalimbali likiwemo la ubadhirifu wa fedha za umma.

Wawili hao wamefunguliwa shauri la jinai namba CC.218/2018 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Hai,Devota Msofe ambako walisomewa maelezo ya mashtaka yao kwa mara ya kwanza.

Katika shauri hilo,Ntakiliho anashtakiwa kwa jumla ya makosa manne ,matatu yakiwa ni ya kughushi na kosa moja la ubadhilifu wa fedha za umma zilizokuwa chini ya uangalizi wake huku Mfanyabiashara Kigumu akishtakiwa kwa makosa mawili.

Shtaka la kwanza linalomkabili mfanyabiashara huyo ni Kughushi nyaraka kuonyesha kwamba kampuni anayomiliki iitwayo Oscar Food and Beverage Catering Service ilipokea shilingi Mil 20,308,000 toka kwa Mkuu wa kitengo cha uchaguzi wilaya ya Hai,Ntakiliho.

Katika nyaraka hizo Kigumu alidai kwamba fedha hizo yalikuwa ni malipo ya chakula na vinywaji kwa ajili ya mafunzo ya wasimamizi wa uchaguzi wa Rais ,Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015 huku akifahamu hajawahi kutoa huduma hiyo.

Shtaka la pili linalomkabili mfanyabiashara huyo ni kumsaidia Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Hai katika uchaguzi mkuu wa Rais ,Wabunge na Madiwani 2015 ,Ntakiliho kufanya ubadhirifu wa Sh Mil 1.495,500.

Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU ,Rehema Mteta aliieleza mahakama kuwa uchunguzi unaonesha kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitenga na kutuma katika jimbo la uchaguzi la Hai,kiasi cha Sh 27,160,00 kwa ajili ya uendeshaji mafunzo ya wasimamizi wa vituo vya uchaguzi. Alieleza kuwa mara baada ya fedha hizo kukabidhiwa kwa Ntakiliho na kufanya matumizi ,alifanya marejesho kwa nyaraka zakughushi kuonyesha kwamba Sh Mil 3,150,000 zilitumika kulipia usafiri wa wawezeshaji wa mafunzo.

Mteta alieleza kuwa Sh Mil 3,702,000 zilitumika kulipia ukodishaji wa ukumbi wa mafunzo na vipaza sauti na Sh Mil 20.308,000 zilitumika kwa ajili ya huduma ya chakula na viburudisho huku akijua kuwa nyaraka hizo zilikuwa za kughushi.

No comments:

Powered by Blogger.